Wanawake wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya uchunguzi wa Saratani ya kizazi inayofanyika katika Kituo cha Afya Likombe kuanzia Agosti 5-7,2021, ili kupata matibabu mapema pale zitakapobainika dalili za ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dkt. Kodi Mohamedi Agosti 5, 2021 wakati wa kuhitimisha mafunzo ya nadharia kwa wahudumu wa Afya watakaotoa huduma hiyo katika Mkoa wa Mtwara.
“Huduma hii ni bure, niwaombe wanawake jitokezeni kwa wingi ili kupata huduma hii na wale watakao bainika kuwa na tatizo aweze kupata matibabu mapema” Amesema Kodi
Ameendelea kusema kuwa aina hii ya saratani inawapata wanawake wenye miaka kati ya 30 hadi 50, wengi wao hawana uelewa wa kutosha juu ya ugonjwa huu hii inapelekea wengi wao kuchelewa kupata matibabu na kuleta athari zaidi baadae.
Naye Meneja kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Maguwa Stephano ameishukuru Bank ya NBC kwa kuratibu zoezi hili, kwa kufanya hivyo Mkoa wa Mtwara umepanua wigo wa kutoa huduma ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa kizazi kutoka vituo 22 hadi kufikia 41.
Kwakuwa Saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kwa kuathiri wanawake wa Mkoa wa Mtwara, Manager wa Bank ya NBC - Mtwara Bw. Emmanuel Mseti amewataka wauguzi hao kutumia elimu hiyo kutatua changamoto hii ya saratani katika Mkoa wa Mtwara.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.