TASAF Yakabidhi Ruzuku Ya Mil.1.8 Kwa Vikundi Vya Kuwekeza na Kuweka Akiba
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga amekabidhi fedha taslimu shilingi milioni 1.800,000 kwa vikundi sita vya kuweka akiba na kuwekeza vilivyopo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini waliopo mtaa wa Chipuputa.
Fedha zilizotolewa ilikuwa ni kutimiza ahadi waliyowaahidi wana vikundi hao baada ya kuwatembelea septemba mwaka jana na kukuta walengwa hao tayari wameshaanza kuweka akiba na kuwekeza kabla mpango huo haujaanzishwa na TASAF.
Akizungumza kwenye mkutano wa kukabidhi fedha hizo uliofanyika Disemba 1 mwaka huu kwenye kiwanja cha mikutano Chipuputa Mwamanga amesema kuwa kutokana na ubunifu waliouonesha wanavikundi hao wa kuuziana sabuni, sukari na vitu vingine waliona ni vema wawaongezee nguvu kwa kuwapa ruzuku itakayoongeza mtaji kwenye mfuko wao wa kuweka akiba na kukopeshana.
Mwamanga amesema kuwa fedha hizo hazina masharti hivyo walengwa waziingize kwenye utaratibu wao wa siku zote kwa kuwa TASAF ina heshimu sana ushirikishwaji wa jamii na mawazo ya Wananchi. Aidha amesema lengo la kuwaongezea fedha hizo ni kuimarisha vikundi na kuwahamasisha watu wajishughulishe ili waweze kuzalisha na kusonga mbele.
Ameongeza kuwa utoaji wa ruzuku haujaishia kwenye vikundi hivyo tayari TASAF imeshakamilisha muundo ambao utashindanisha vikundi vinavyoweka akiba na kuwekeza na kikundi kitakachofanya vizuri kitaongezewa ruzuku ili viendelee kuwa vizuri zaidi.
Amesema kuwa hadi sasa TASAF imeweza kuwafikia walengwa kwa asilimia 70 ya Mitaa, vijiji na sheia kwa Zanzibar na kwamba lengo la Serikali ni kumaliza asilimia 30 ya sehemu zilizobaki hivyo hadi kufikia mwakani mpango wa pili wa TASAF 111 ambao sasa unaandaliwa utakuwa umekamilika.
Akizungumzia kuhusu ucheleweshaji wa malipo ya ajira za muda amesema kuwa tatizo kubwa ilikuwa ni mfumo ambapo kama taarifa za waliofanya kazi ya ajira za muda hazijaingiizwa kwenye mfumo huwezi kulipa hadi halmshauri zote ziwe zimeshaingiza lakini TASAF imekubaliana na wadau wa Maendeleo na Serikali kuwa kama sehemu imechelewa kuingiza taarifa wengine wasicheleshwe malipo
Ameongeza kuwa kwa wanafunzi waliopo kwenye kaya za mpango na hawakubahatika kuchaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari TASAF bado inawaangalia na wanaweza kusaidiwa ada kujiunga kwenye ufundi pamoja na fedha ya kujikimu kwenye majukumu mengine kama ununuzi wa nguo n.k..Na kwa watu wenye ulemavu ambao hawawezi kufanya kazi za ajira za muda TASAF itaangalia namna nzuri ili na wao waweze kunufaika.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Ernest Mwongi amewashukuru TASAF kwa juhudi wanazozifanya kwa kuwasaidia Wananchi kwani imepunguza mzigo kwa halmashauri kwa kuwa kuna mambo mengine yalitakiwa yafanywe na Manispaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Chipuputa Hamisi Chambea ameshukuru kwa mtaa wake kufikiwa na TASAF na wananchi wake wamenufaika na ajira za muda na wamejenga mifereji na kwamba wao kama viongozi wako imara katika kuusimamia mradi.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika Mtaa wa Chipuputa Afisa mtendaji wa Mtaa huo Henry Lupapa amesema kuwa Chipuputa ina walengwa 118 ambao wananufaika na mpango..Amesema kuwa shilingi milioni 81,160,230 zimehaulishwa kuanzia kipindi cha Machi-April 2014 hadi sasa, na jumla ya awamu 23 za malipo zimefanyika. Pia jumla ya shilingi 25, 944,400 zimehaulishwa kupitia miradi ya ajira za muda kuanzia mwezi Januari 2015 hadi sasa. Vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza vilivyopata ruzuku ni pamoja na kikundi cha Amani, Imani, Hapa kazi, Azimio, kubali na ushirikiano na kila kikundi kimepata ruzuku ya shilingi 300,000.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.