Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe: Gelasius G. Byakanwa akizindua zoezi la Uandikishaji Daftari la Wakazi Kimkoa lililofanyika kwenye Viwanja vya Ofisi ya Kata Shangani
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe: Gelasius Byakanwa ametoa muda wa miezi mitatu kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara kujiandikisha kwenye daftari la wakazi lililopo kwenye kila Mtaa.
Amesema kuwa kama muda huo utapita na mwananchi hajajiandikisha kwenye daftari hilo hatatoa adhabu yeyote, badala yake mwananchi atakosa huduma mbalimbali kutoka kwenye Ofisi za Serikali ikiwemo barua za utambulisho zinazotakiwa kwenye mabenki na huduma zingine..
Byakanwa amezungumza hayo leo wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uandikishaji kwenye daftari la wakazi Kimkoa lililofanyika kwenye Viwanja vya Ofisi ya Kata Shangani Manispaa Mtwara-Mikindani. Aidha amewataka watendaji kutomkaribisha mgeni yeyote kwenye Mtaa kama hana taarifa za kujiandikisha kwenye mtaa alikotokea.
Amesitiza kuwa ili kuendelea kulinda amanii, utulivu na kuondoa uhalifu kwenye maeneo yao ni lazima wananchi wakafahamiana kwa kujiandikisha kwenye daftari la wakazi linalomilikiwa na Mtendaji wa Mtaa. Pia ameagiza mtu yeyote anapohamia kwenye mtaa ni lazima ajiandikishe kwenye daftari hilo ili taarifa zake zingizwe.
Mkuu huyo wa Mkoa amezitaja faida zitokanazo na wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wakazi kuwa ni pamoja na kusaidia Serikali kupanga bajeti ,mahitaji ,na huduma za jamii kwa watu wake kwa kuwa takwimu za idadi ya watu waliopo kwenye mitaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi Taifa zitakuwepo. Faida zingine ni pamoja na kuimarisha Ulinzi na Usalama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Bi Beatrice Dominic amesema kuwa kutokana na uelewa mdogo wa wananchi juu ya zoezi hili, imepelekea idadi ya waliosajiliwa kwenye daftari la wakazi kwa Manispaa kuwa ndogo na kufikia watu 46,704 Kati ya Wakazi 115,114 wanaokadiriwa kuwepo kwenye Manispaa. Aidha amesema kuwa anatarajia baada ya uzinduzi huo wananchi watatimiza wajibu wao kwa kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Ameongeza kuwa Daftari hilo litatunzwa na Mwenyekiti wa Mtaa husika na kwamba Mwenyekiti atapaswa kujaza fomu kila taarifa mpya zinapojitokeza zikiwemo vizazi,Vifo, kuhama na kuhamia. Aidha kazi za Mtendaji wa Mtaa ni kuhakikisha daftari linaingizwa Taarifa, linatunzwa na linatumika.
Daftari la wakazi lipo kisheria chini ya sheria ya Serikali za Mitaa Na. 6 ya mwaka 1982, na limechapishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI mwaka 2011.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.