Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara Mjini Mhe. Salumu Mpilu amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-mikindani Col. Emanuel Mwaigobeko kwa usimamizi wa miradi ya Maendeleo inayotekelezwa ndani ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
"Niseme tu wazi Mkurugenzi umejitahidi sana, lengo la ziara ni kuja kukagua miradi na sisi tulita kuja kuona sio kusimuliwa na tumejionea , hongera sana " amesema Mpilu
Mhe. Mpilu ametoa pongezi hizo Agosti 10,2021 katika ziara ya Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mtwara Mjini ilipotembelea miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ndani ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na amemtaka Mkurugenzi kuendelea na kasi hiyo ili miradi iweze kukamilika kwa wakati.
Aidha katika ziara hiyo Mhe. Mpilu ameonesha kufurahishwa na ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo yao na kuwataka wananchi hao kushirikiana na Serikali katika kuilinda miradi hiyo pindi itakapomalizika.
"Nimefurahi kusikia nguvu za wananchi katika miradi hii, nikuombe Mkurugenzi washirikishe kwenye kuilinda pia maana ni jasho hili, nguvu zao zisiende bure" amesema Mhe. Mpilu
Katika ziara hiyo kamati ya siasa imefanikiwa kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo la X-ray katika Kituo cha afya Likombe, Ujio wa chujio la maji Mangamba Chini, Ujenzi wa Zahanati na nyumba ya mtumishi Mbawala Chini pamoja na ujenzi wa mwalo na choo katika eneo la Kata ya jangwani iliyopo Mikindani.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.